Na
Zahara Tunda
Ikiwa tarehe 11
Octoba ni siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani; wawakilishi wa Asasi za Kiraia wameungana na
wadau wa elimu, afya na nyanja nyingine zote na jamii kwa ujumla kuiomba serikali
kuwekeza zaidi katika elimu ya mtoto wa kike.
Uwekezaji huu uendane na
dhamira thabiti ya kulinda haki za mtoto wa kike na kumuondolea vizuizi katika
elimu. Vilevile kuona hatua za makusudi katika kupambana na ndoa na mimba za
utotoni, watoto wa kike kukatisha masomo na aina zote za unyanyasaji wa
kijinsia.
|
Greysmo Mutashobya meneja miradi -Health Promotion Tanzania |
“Kwa pamoja tunatoa wito kwa kusema ondoa vizuizi vya
kijamii, kitamaduni, na vile vya kimiundombinu ili kufanikisha usawa katika
elimu ya sekondari na chuo kwa mtoto wa kike.” Alisema
Greysmo Mutashobya meneja miradi wa Health Promotion Tanzania.
Hali halisi ya changamoto ya mtoto kwa mujibu wa takwimu
ya hesabu ya watu duniani ya mwaka 2017 (The world population countdown)
inaonesha kuwa wasichana wenye umri kati ya miaka 10 na 19 ni takribani milioni
600 ulimwenguni kote.
Kwa Tanzania wasichana wa umri huo ni takribani
asilimia 18 ya watanzania wote. Ripoti
ya maendeleo ya serikali kwa mwaka 2016 ilionyesha kuwa idadi ya udahili wa
wasichana kwa shule za msingi ilizidi ile ya wavulana kwa asilimia 0.1.
Vyanzo vingine vinaonesha kuwa wasichana 550,000
walikatishwa masomo yao baada ya kupata ujauzito katika kipindi cha muongo
mmoja uliopita. Wasichana wanakuwa wazazi na walezi katika umri mdogo na hii inaathiri
sio maisha yao tu bali hata familia zao, watoto wao na taifa kwa ujumla.
Takwimu za (TDHS-MIS) kwa mwaka 2015-16 zinaonyesha
kuwa asilimia 27 ya wakina mama wote waliojifungua walikuwa wasichana chini ya
miaka 20.
Pia, takwimu zionesha kuwa msichana mmoja (15-19) kati
ya watano ana angalau mtoto mmoja na wasichana wanne (miaka 20-24) kati ya kumi
nao angalau wamejifungua mara moja kabla ya kufikia miaka 18; hali hii hujitokeza
sana maeneo ya vijijini ukilinganisha na mjini. Hii haimaanishi mjini pako
salama, la hasha.
Hivyo basi, ni vema kutambue kuwa mila na desturi
nyingine ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya mtoto wa kike na tuzipinge kwa
nguvu zote.
Mila ambazo mpaka sasa zimeonekana hatarishi ni pamoja
na: ndoa za utotoni, ukeketaji, ubaguzi wa kijinsia na upendeleo kwa jinsia ya
kiume, mfumo dume na nyingine za aina hii.
Mila hizi zinabinya haki ya mtoto wa kike kupata
taarifa na huduma rafiki za afya na matokeo yake ni kuongezeka kwa mimba za
utotoni, vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na umasikini wa kipato kwa
ngazi ya familia.
|
Pamela Marssay Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki |
“Wanawake tusimame vifua mbele kuwahamasisha watoto
wakike ,kuwatia moyo katika kufikia malengo yao “ alisema Bi Pamela Marssay
mbunge wa bunge la Afrika Mashariki.
Aliendelea kwa kusema “Asasi zote za kiraia na watu nyanja
mbalimbali inapaswa tupaze sauti kila mmoja wetu apaze sauti ili tupate sera na
sheria zitakazo msaidia mtoto wa kike”
Asasi hizi wameiomba serikali kutengeneza mazingira ya
usawa na wezeshi ambayo yataweza kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike. Jambo
hili liendane na kuondoa vizuizi katika elimu kwa mtoto wa kike;
Vilevile serikali
ifanye mapitio ya Sheria na Sera ili kufanya mabadiliko ya Sera na Sheria
zinazopalilia mila potofu, unyanyasaji na ndoa za utotoni;
Aidha wameiomba serikali iharamishe ndoa za utotoni na
ichukue hatua za haraka kubadilisha Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu
ndoa katika umri wa miak 14; tunapendekeza umri wa ndoa uwe miaka 18 kwa wasio
wanafunzi.
Pia wametoa wito kwa wazazi kuchukua hatua na
kuzingatia malezi bora na yenye tija kwa mtoto wa kike; wazazi wawe mstari wa
mbele kuondoa dhana ya upendeleo wa kijinsia.
Mwisho kabisa wametoa wito kwa mtoto wa kike kupambana
na changamoto na azishinde, abadili mtazamo wake, apinga ndoa za utotoni, awe
mvumilivu na asiingie katika mahusiano ya kimapenzi kabla ya wakati wako.“ Tulizana shuleni ijenge kesho yako.”