Wednesday, 11 October 2017

ASASI ZA KIRAIA ZAIOMBA SERIKALI KUDUMISHA ELIMU YA MTOTO WA KIKE



Na Zahara Tunda
Ikiwa tarehe 11 Octoba ni siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani;  wawakilishi wa Asasi za Kiraia wameungana na wadau wa elimu, afya na nyanja nyingine zote na jamii kwa ujumla kuiomba serikali kuwekeza zaidi katika elimu ya mtoto wa kike.
Uwekezaji huu uendane na dhamira thabiti ya kulinda haki za mtoto wa kike na kumuondolea vizuizi katika elimu. Vilevile kuona hatua za makusudi katika kupambana na ndoa na mimba za utotoni, watoto wa kike kukatisha masomo na aina zote za unyanyasaji wa kijinsia.


Greysmo Mutashobya meneja miradi -Health Promotion Tanzania

“Kwa pamoja tunatoa wito kwa kusema ondoa vizuizi vya kijamii, kitamaduni, na vile vya kimiundombinu ili kufanikisha usawa katika elimu ya sekondari na chuo kwa mtoto wa kike. Alisema Greysmo Mutashobya meneja miradi wa Health Promotion Tanzania.

Hali halisi ya changamoto ya mtoto kwa mujibu wa takwimu ya hesabu ya watu duniani ya mwaka 2017 (The world population countdown) inaonesha kuwa wasichana wenye umri kati ya miaka 10 na 19 ni takribani milioni 600 ulimwenguni kote.
Kwa Tanzania wasichana wa umri huo ni takribani asilimia 18 ya watanzania wote.  Ripoti ya maendeleo ya serikali kwa mwaka 2016 ilionyesha kuwa idadi ya udahili wa wasichana kwa shule za msingi ilizidi ile ya wavulana kwa asilimia 0.1.
Vyanzo vingine vinaonesha kuwa wasichana 550,000 walikatishwa masomo yao baada ya kupata ujauzito katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Wasichana wanakuwa wazazi na walezi katika umri mdogo na hii inaathiri sio maisha yao tu bali hata familia zao, watoto wao na taifa kwa ujumla.

Takwimu za (TDHS-MIS) kwa mwaka 2015-16 zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wakina mama wote waliojifungua walikuwa wasichana chini ya miaka 20.
Pia, takwimu zionesha kuwa msichana mmoja (15-19) kati ya watano ana angalau mtoto mmoja na wasichana wanne (miaka 20-24) kati ya kumi nao angalau wamejifungua mara moja kabla ya kufikia miaka 18; hali hii hujitokeza sana maeneo ya vijijini ukilinganisha na mjini. Hii haimaanishi mjini pako salama, la hasha. 
Hivyo basi, ni vema kutambue kuwa mila na desturi nyingine ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya mtoto wa kike na tuzipinge kwa nguvu zote.
Mila ambazo mpaka sasa zimeonekana hatarishi ni pamoja na: ndoa za utotoni, ukeketaji, ubaguzi wa kijinsia na upendeleo kwa jinsia ya kiume, mfumo dume na nyingine za aina hii.
Mila hizi zinabinya haki ya mtoto wa kike kupata taarifa na huduma rafiki za afya na matokeo yake ni kuongezeka kwa mimba za utotoni, vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na umasikini wa kipato kwa ngazi ya familia.

Pamela Marssay Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki


“Wanawake tusimame vifua mbele kuwahamasisha watoto wakike ,kuwatia moyo katika kufikia malengo yao “ alisema Bi Pamela Marssay mbunge wa bunge la Afrika Mashariki.
Aliendelea kwa kusema “Asasi zote za kiraia na watu nyanja mbalimbali inapaswa tupaze sauti kila mmoja wetu apaze sauti ili tupate sera na sheria zitakazo msaidia mtoto wa kike”
Asasi hizi wameiomba serikali kutengeneza mazingira ya usawa na wezeshi ambayo yataweza kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike. Jambo hili liendane na kuondoa vizuizi katika elimu kwa mtoto wa kike;
 Vilevile serikali ifanye mapitio ya Sheria na Sera ili kufanya mabadiliko ya Sera na Sheria zinazopalilia mila potofu, unyanyasaji na ndoa za utotoni;
Aidha wameiomba serikali iharamishe ndoa za utotoni na ichukue hatua za haraka kubadilisha Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu ndoa katika umri wa miak 14; tunapendekeza umri wa ndoa uwe miaka 18 kwa wasio wanafunzi.
Pia wametoa wito kwa wazazi kuchukua hatua na kuzingatia malezi bora na yenye tija kwa mtoto wa kike; wazazi wawe mstari wa mbele kuondoa dhana ya upendeleo wa kijinsia.
Mwisho kabisa wametoa wito kwa mtoto wa kike kupambana na changamoto na azishinde, abadili mtazamo wake, apinga ndoa za utotoni, awe mvumilivu na asiingie katika mahusiano ya kimapenzi kabla ya wakati wako.“ Tulizana shuleni ijenge kesho yako.”


No comments:

Post a Comment

USALAMA WA WATOTO BARABARANI UTAZAMWE TENA

Kila mzazi au mlezi mwenye mtoto ni jukumu lake kuhakikisha usalama wa mtoto wake hasa aendapo shuleni na kurudi. Hii ni kutokana na maen...